Leo tarehe 7 Januari ni siku ya kuzaliwa ya mwigizaji wa filamu za Nigeria Yul Edochie na mke wake wa pili Judy Austin amemwandikia ujumbe mtamu.
Yul ametimiza umri wa miaka 43 na Judy anajirejelea kama mwanamke mwenye bahati zaidi kwa kuwa na mume kama Yul huku akichapisha picha zake.
Judy ambaye ana watoto wawili wa kiume na Yul, amesema sio sadfa kwamba siku yake ya kuzaliwa inajiri wiki moja tu baada ya ile ya Yul, akimtaja kuwa baraka kubwa kwa maisha yake.
Kutokana na hilo anasema utangamano wao ni wa kipekee na ndio nguvu yao ya pamoja. ” Asante kwa kunifanya bora na thabiti mpenzi.” aliandika mwigizaji huyo.
Aliendelea kummiminia sifa akisema yeye ni mume wa kutegemewa, mwanaume mwenye nguvu, asiyeogopa lolote na ambaye anatosha.
Ndoa ya wawili hao hata hivyo imekuwa ikikashifiwa na wengi nchini Nigeria kutokana na lalama za mke wa kwanza wa Yul Edochie, May Edochie, ambaye alisema kamwe hataki kuwa kwenye ndoa ya wake zaidi ya mmoja.
Tetesi zinaarifu kwamba May ameanzisha mchakato wa talaka.