Mwanamuziki wa mtindo wa Genge nchini Kenya Jua Cali anaendelea kupata nafuu baada ya kuugua na hata kulazwa hospitalini.
Alichapisha picha kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa ameketi nyumbani akisema anapumzika tu.
Yapata wiki moja iliyopita mke wa Jua Cali aitwaye Lilian alichapisha picha inayomwonyesha Cali akiwa kwenye kitanda cha hospitali naye akiwa kando yake huku akimtakia afueni ya haraka.
Wawili hao hata hivyo hawakuweka wazi alichokuwa akiugua Jua Cali ambacho kilisababisha aahirishe tamasha alilokuwa amepanga.
Baada ya siku chache alichapisha picha nyingine akiwa nyumbani akielezea kwamba alikuwa ameruhusiwa kuondoka hospitalini.
“Watu wangu niko nyumbani najihisi bora, niliondoka hospitalini.” aliandika mwanamuziki huyo huku akishukuru Mungu, ndugu, jamaa na marafiki waliosimama naye akiwa amelazwa.
Msanii huyo alishukuru pia wahudumu wa hospitali ambayo alikuwa amelazwa ya Mp Shah kama daktari na wauguzi ambao alisema walimshughulikia vyema.
Alifichua pia kwamba anachukua mapumziko kutoka kwa kazi zake kama msanii akiendelea kupata nafuu.