Hukumu dhidi ya Jowie kutolewa Jumatano ijayo

Martin Mwanje
1 Min Read

Joseph Irungu almaarufu Jowie atafahamu kifungo atakachotumikia gerezani Jumatano wiki ijayo, saa tano na nusu asubuhi.

Hii ni baada ya awali Jaji Grace Nzioka kumpata na hatia ya kumuua mfanyabiashara Monica Kimani.

Jaji Nzioka alilazimika kuaihirisha utoaji wa hukumu dhidi yake leo Ijumaa baada ya stakabadhi muhimu ambazo zingesaidia katika kutolewa kwa hukumu hiyo kuchelewa kuwasilishwa kwake.

Kuaihirishwa huko pia kuliripotiwa kuchangiwa na hatua ya Jowie kumbadilisha mwanasheria wake.

Mwanasheria wa Jowie aliiambia mahakama kwamba alihitaji muda wa wiki moja kupitia hukumu iliyompata Jowie na hatia ya kumuua mfanyabiashara Kimani na kujibu, ombi ambalo mahakama ilikataa.

Kwa hivyo jaji Nzioka aliagiza kwamba majibu yawasilishwe kufikia Jumanne wiki ijayo ili atoe hukumu hiyo Jumatano.

Jowie alitarajiwa siku ya Ijumaa Machi 8 kuhukumiwa baada ya kupatikana na kosa la mauaji mwezi Februari mwaka huu.

Mwanahabari Jackie Maribe ambaye alikuwa ameshtakiwa na Jowie aliachiliwa huru baada ya upande wa mashtaka kukosa ushahidi kamili wa kumhusisha Maribe na mauaji hayo.

Hata hivyo, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga aliwasilisha ilani mahakamani akielezea nia ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Share This Article