Jopokazi la kushughulikia mizozo ya ardhi Nairobi lazinduliwa

Tom Mathinji
4 Min Read

Jaji Mkuu Martha Koome leo Jumanne alizindua jopokazi litakaloshughulikia kesi za mashamba katika Kaunti ya Nairobi.

Jopokazi hilo linajumuisha washikadau kutoka sekta ya haki kuhusu ardhi.

Limepewa jukumu la kutambua vyanzo vinavyosababisha changamoto za kupata haki katika kesi za mashamba na kushughulikia changamoto za kimfumo.

Jopokazi hilo linatarajiwa kuhusisha umma na washikadau katika juhudi za kutafuta suluhu za kudumu kwenye kesi za mashamba kwa minajili ya kukuza mustakabali wa usawa siku za usoni.

Kadhalika linatarakiwa kupendekeza hatua mahususi, kubuni mwongozo utakaotumiwa kuharakisha utoaji wa haki kwenye kesi za mashamba kupitia ukumbatiaji wa mbinu bora za kupata haki zikiwemo mifumo mbadala ya haki na usuluhishi ulioambatanishwa na mahakama.

Jaji Koome alisema kuwa jukumu lake litaambatana na malengo ya kubadilisha jamii kupitia upatikanaji wa haki, hususan kupunguza muda wa kesi ili usizidi miaka mitatu.

Alisema jopokazi hilo litachunguza vyanzo vinavyosababisha kucheleweshwa kwa kesi na kurahisisha michakato ya usimamizi wa kesi na kupitisha mbinu bunifu za utoaji haki.

Koome alibainisha kuwa hayo yataharakisha utatuzi wa kesi za mashamba, kupunguza mrundiko na ufumbuzi wa kudumu wa kupunguza changamoto za haki ya kesi za mashamba.

Aliongeza kuwa kubuniwa kwa jopokazi la kushughulikia haki za kesi za mashamba ni dhihirisho la kujitolea kwa mahakama ya Mazingira na Ardhi katika kuharakisha kutolewa kwa haki za kesi za mashamba jijini Nairobi.

“Mpango huu si wa kawaida, unakusudia kukuza mfumo wa haki ambao ni jumuishi, shirikishi, unaowajibika, na sikivu ambao kwa kweli unatimiza matarajio ya watu wetu, ikiwa ni pamoja na wale waliotengwa na walio hatarini zaidi miongoni mwetu,” alisisitiza Koome.

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu.

Akipongeza juhudi za mahakama ya mazingira katika kushughulikia haki za kesi za mashamba, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alisema kuwa atafuatilia kwa makini kazi ya jopokazi hilo ili kulitumia kama kielelezo kabla ya kuanzisha majopokazi mengine kwenye kaunti zingine na maeneo ya mamlaka ya mahakama.

Alihimiza jopokazi hilo kushirikisha mfumo wa usimamizi wa utendaji utakaowawezesha kufuatilia na kuboresha utendaji wao na kupata matokeo yanayoonekana.

Katika hotuba yake, Waziri wa Ardhi Alice Wahome aliahidi kuunga mkono kuhakikisha malengo ya jopokazi hilo yanafikiwa na haki ya ardhi inafikiwa ili kuokoa watu, hasa wazee dhidi ya dhuluma.

Kaunti ya Nairobi inakumbwa na masuala ya ugawaji maradufu wa ardhi, uvamizi wa ardhi ya umma, michanganyiko wakati wa upimaji, madai mabaya ya umiliki, ukosefu wa ukandaji na utekelezaji, makazi yasiyo rasmi, upangaji upya wa ukodishaji na udanganyifu na hivyo kuunda mtandao tata wa dhuluma ya ardhi ambayo ni vigumu kusafiri nje ya mbinu ya ushirikiano wa sekta nyingi.

Jopokazi hilo ambalo ni chanzo cha Kamati ya Watumiaji wa Mahakama ya Nairobi inatoa uanachama wake kutoka ELC, Kaunti ya Nairobi, Wizara ya Ardhi, Mwanasheria Mkuu, Tume ya Kitaifa ya Ardhi na Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa miongoni mwa zingine.

 

TAGGED:
Share This Article