Jopo la uteuzi wa IEBC laongezewa muda wa kuhudumu

Jopo hilo limeongezewa siku 14 zaidi ili kukamilisha usaili, kuteua wanaofaa na kuwasilisha majina kwa Rais.

Marion Bosire
1 Min Read
Dkt. Nelson Makanda, Mwenyekiti wa jopo la uteuzi wa IEBC

Bunge la taifa limeongeza muda wa kuhudumu wa jopo la uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa tume ya uchaguzi na uratibu mipaka nchini IEBC kwa siku 14 zaidi.

Haya yanafuatia mjadala wa hoja iliyotolewa na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed aliyesema kwamba kufuatia mpangilio wa usaili wa wawaniaji wa nyadhifa hizo, jopo hilo haliwezi kukamilisha mchakato huo kwa muda uliowekwa awali.

Kulingana na sheria, jopo hilo lilikuwa limepatiwa siku 90 kukamilisha usaili na kuwasilisha majina ya walioteuliwa kwa Rais kwa ajili ya uteuzi rasmi.

Wanachama wa jopo la uteuzi waliapishwa na jaji mkuu Martha Koome Januari 27, 2025 na wakaanzisha mchakato wa usaili Jumatatu Machi 24, 2025 kwa wanaomezea mate wadhifa wa mwenyekiti.

Hatua hii iliwezeshwa na kuondolewa kwa amri  ya awali ya mahakama iliyokuwa inazuia mchakato huo na mahakama kuu Ijumaa Januari 24, 2025.

Jopo hilo chini ya uenyekiti wa Dr. Nelson Makanda kwa sasa linaendeleza usaili wa wanaotaka kuwa makamishna wa IEBC.

Jumla ya watu 105 waliorodheshwa kuwania nyadhifa sita za makamishna huku 11 wakisailiwa kwa wadhifa wa mwenyekiti.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *