Jaji Mkuu Martha Koome anatarajiwa kubuni jopo la majaji watakaosikiliza kesi ya kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hii inafuatia ombi lililotolewa na timu ya wanasheria wa Gachagua juzi Jumatano, ikiongozwa na mwanasheria mwandamizi Paul Muite.
Katika ombi lake, timu hiyo ilimtaka Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi kuwasilisha kesi dhidi ya Gachagua kwa Jaji Mkuu ili abuni jopo la majaji kati ya watatu hadi saba watakaosikiliza kesi ya kupinga kubanduliwa madarakani kwa Naibu wa Rais.
Jaji Mugambi ameitikia uamuzi huo leo Ijumaa asubuhi.
“Hii ni moja ya matukio adimu ambapo mahakama inapaswa kuchukua uongozi na kuhudumia umma kwa kutumia rasilimali zote inazoweza kutumia,” amesema Jaji Mugambi katika uamuzi wake.
“Kwa mtazamo wangu, licha ya pingamizi kali kutoka kwa washtakiwa, ni maoni yangu kwamba kesi hizi zinaibua masuall mazito ya kikatiba kwa mujibu wa kifungu 165 (3) (b) na (d)(ii) cha katiba na kwa hivyo, nimeshawishika kuzielekeza kwa Jaji Mkuu kubuni jopo la kuzikiliza.”
Jumla ya kesi 6 zilizowasilshwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa zitaelekezwa kwa Jaji Koome ili kutoa mwelekeo katika kubuni jopo la majaji wa kuzisikiliza huku zikitarajiwa kujumishwa.
Kati ya kesi hizo, kesi E522,2024 imetajwa kuwa kinara.
Wabunge 281 Jumanne wiki hii waliunga mkono hoja ya kutimuliwa kwa Gachagua iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Bunge la Seneti linatarajiwa kuzingatia hoja hiyo Jumatano na Alhamisi wiki ijayo huku Naibu Rais akitarajiwa kufika mbele ya bunge hilo kujitetea.
Ikiwa Seneti itaridhiana na bunge la Taifa na kupitisha hoja hiyo, basi Gachagua atabanduliwa rasmi kwenye wadhifa huo.
Hata hivyo, huenda akapata afueni katika mahakama ikiwa agizo litatolewe la kuzuia kutimuliwa kwake hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani isikizwe na kuamuliwa.