Jopo kazi kuhusu chuo kikuu Trans Nzoia lakamilisha uchunguzi

Marion Bosire
1 Min Read

Jopo lililobuniwa na Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya kuongoza shughuli ya kuanzisha chuo kikuu cha kaunti limemaliza kazi.

Kulingana na Naibu mwenyekiti wa jopo hilo Daktari Hellen Yego, wamemaliza kazi waliyopatiwa na wako tayari kumkabidhi Gavana ripoti yao.

Aizungumza na wanahabari Jumamosi mjini Kitale, Yego alisema ripoti yao inajumuisha maoni ya wakazi wa kaunti hiyo hata wanaofanya kazi ughaibuni.

Jopo kazi hilo lilishirikisha pia wataalamu na wadau mbali mbali wa sekta ya elimu ili kuhakikisha ripoti kamilifu.

Kennedy Etyang afisa mkuu wa elimu katika serikali ya kaunti ya Trans Nzoia amepongeza jopo kazi hilo kwa kujitolea na kuvumilia changamoto nyingi.

Etyang anahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kwamba serikali ya Natembeya itatekeleza mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo punde itakapowasilishwa.

Kulingana naye, kaunti ya Trans Nzoia iko tayari kabisa kwa awamu ya pili ya mpango mzima wa kuanzisha chuo kikuu.

Afisa huyo mkuu wa elimu alisema kaunti hiyo inahitaji sana taasisi ya elimu ya juu ndoto ambayo anasema itatimia.

Jopo hilo la utafiti kuhusu kuanzishwa kwa chuo kikuu cha kaunti ya Trans Nzoia lilibuniwa Aprili 16, 2023.

Limekuwa likizuru vyuo vikuu vilivyo karibu kwa ajili ya kujifahamisha kikiwemo chuo kikuu cha Eldoret.

Share This Article