Jomo, mwanawe Rais Uhuru Kenyatta aondoa kesi dhidi ya serikali

Marion Bosire
1 Min Read

Jomo Kenyatta mwanawe aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta ameondoa kesi dhidi ya serikali ambapo alikuwa ameishtaki kwa kutaka kumpokonya bunduki zake kwa kufutilia mbali leseni ya kuzimiliki.

Wakili wa Jomo kwa jina Fred Ngatia ndiye aliondoa kesi hiyo mahakamani na sasa inamaanisha kwamba mtoaji leseni za kumiliki silaha nchini hatahitilafiana na leseni ya Jomo.

Jaji Jairus Ngaah ndiye aliidhinisha mapatano kati ya Jomo na bodi ya kutoa leseni za kumiliki silaha nchini.

Jomo alielekea mahakamani mwaka jana baada ya makazi yake kuvamiwa na watu waliojitambulisha kama maafisa wa polisi.

Kupitia kwa wakili wake, Jomo aliambia mahakama kwamba leseni yake ilikuwa inatumika hadi Aprili 2024.

Watu hao wanasemekana kuagiza waliokuwa kwenye makazi ya Jomo kusalimisha bunduki zilizokuwa huko.

Mwezi Disemba mwaka jana, Jomo aliambia jaji Ngaah kwamba yeye na bodi ya kutoa leseni za kumiliki bunduki wamekuwa wakishauriana ili kutatua suala hilo nje ya mahakama.

Leo Januari 31, 2024, wahusika wa kesi hiyo walifika mahakamani kufahamisha jaji kuhusu hatua walizopiga katika mashauriano hayo.

Website |  + posts
Share This Article