Joho abuni kamati ya kutatua utata wa TATA

Kamati hiyo ilibuniwa siku moja baada ya Waziri Joho kuishtumu kuwa imekiuka sheria za Kenya kuhusu operesheni za uchimbaji madini.

Tom Mathinji
1 Min Read
Hassan Joho - Waziri wa Madini.

Waziri wa Madini Hassan Joho amebuni kamati ya kiufundi kushughulikia utata unaoghubika kampuni ya Tata Chemicals Magadi Limited.

Kupitia kwa taarifa Jumanne usiku, Joho alitangaza kuwa kamati hiyo itaongozwa na Katibu katika Wizara ya Madini Harry Kimtai kwa niaba ya serikali ya Kenya na Swaminathan Nagarajan ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Tata.

Kamati hiyo ilibuniwa siku moja baada ya Joho kuishutumu kuwa imekiuka sheria za Kenya kuhusu operesheni za uchimbaji madini.

Miongoni mwa maswala ambayo kamati hiyo imejukumiwa kushughulikia ni pamoja na manufaa ya kijamii yanayotokana na shughuli za kampuni hiyo, mzozo wa ardhi ambao haujashughulikiwa, upanuzi wa eneo hilo kwa shughuli za uchimbaji madini, na maswala yanayohusiana na serikali ya kaunti ya Kajiado ambayo hayajatatuliwa.

“Kama serikali, tumejitolea kushirikiana na wawekezaji kwa kuzingatia sheria za Kenya na manufaa ya raia wake,” alisema Joho.

Aidha, Waziri huyo alifafanua kwamba hatua hiyo hailengi tu kutatua masuala ya uzingatiaji sheria, lakini pia inanuia kubuni mkakati endelevu unaokuza uchimbaji madini unaowajibika, uongezaji thamani, manufaa ya kijamii na ushirikiano unaofaidi pande mbili.

Kulingana na Joho, Kenya  inapaswa kunufaika kiuchumi kutokana na maliasili yake kupitia ushiriki wa wananchi kwa shughuli za uchimbaji madini.

Share This Article