John Dumelo amwomboleza babake

Mwigizaji huyo wa Ghana alitangaza kifo cha babake mzazi kupitia Instagram, akielezea kwamba aliaga dunia muda mfupi baada ya kuzungumza naye.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa Ghana John Dumelo amemwomboleza babake Mhandisi John William Kudzo Anato-Dumelo Snr.

John ambaye pia ni mwanasiasa na mbunge mteule wa eneo bunge la Ayawaso West Wuogon alichapisha picha ya pamoja akiwa na babake na kuelezea kwamba ameaga akiwa na umri wa miaka 75.

Alielezea kwa kirefu muda alionana naye akiwa hai asijue ndio wakati wake wa mwisho ulimwenguni.

“Jana ulinipigia simu mara kadhaa ukitaka nije nikuone. Tuliketi kitandani tukazungumza kwa kina kuhusu siasa, maisha, kilimo, biashara na hata umbea.” aliandika mwigizaji huyo ambaye pia hujihusisha na kilimo.

Aliendelea kueleza jinsi walijadili uapisho wake ujao na baba akamshauri ahudumu vyema serikalini. “Dakika kumi baada ya kuondoka nyumbani kwako nilipigiwa simu kwamba hauitiki.” aliandika Dumelo.

Kulingana naye, alirejea kwa babake akampeleka hospitalini ambapo alifahamishwa kwamba alikuwa amekata roho. Alimshukuru kwa kuwa babake, rafiki wa dhati, mshangiliaji wake na kwa kila kitu aliwahi kumfanyia maishani.

Kifo cha babake John Dumelo kinajiri mwaka mmoja na miezi kadhaa baada ya mamake kuaga dunia. Mama Antoinette Dumelo aliaga dunia Agosti 15, 2023.

John alichaguliwa mbunge katika uchaguzi mkuu wa hivi maajuzi nchini Ghana na hiyo ilikuwa mara ya pili kwake kuwania wadhifa huo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *