Mwanamuziki wa Uganda John Blaq ameonya mashabiki na vyombo vya habari kuhusu usiri wa maisha yake hasa katika masuala ya mapenzi.
Blaq ambaye jina lake halisi ni John Kasadha alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alishangaa ni kwa nini mashabiki na vyombo vya habari hufuatilia maisha yake sana.
“Nataka maisha yangu yawe ya faragha kwa sababu mimi pia sina haja na kinachoendelea kwenye maisha yenu” alisema mwanamuziki huyo.
Lakini alipoulizwa iwapo kwa sasa ana mpenzi Blaq hakutoa jibu mwafaka akisema kwamba hata ingawa hajatangaza rasmi huenda mpenzi yuko.
Aliongeza kusema kwamba yeye ni mwanaume anayependa wanawake sana na anataka afahamike hivyo ili kuweka mbali uwezekano wa kudhaniwa kuwa shoga.
“Huwa ninajaribu sana kuonekana kama mwanaume anayependa wanawake. Sitaki kamwe kuhusishwa na mashoga kwa njia yoyote ile” alisema Blaq.
Msanii huyo aliendelea kwa kukiri kwamba bado hajapata mpenzi ambaye atatangazia umma na hata ingawa ana mtu, wakati wa kumtangaza bado haujawadia.
“Kila kitu kina muda wake” alisema.
Penzi linalofahamika la John Blaq ni kati yake na mwanamuziki Vanessa, ambaye ni mzazi mwenza wa mwanamuziki Ziza Bafana. Video yao iliwahi kusambaa mitandaoni ikiwaonyesha wakiwa pamoja.