Jinamizi la utekaji nyara lazima likomeshwe, asema Kalonzo

Martin Mwanje
1 Min Read
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka akiwahutubia wanahabari akiwa ameandamana na viongozi wengine wa upinzani

Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema kuna haja ya serikali kukomesha mara moja visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara nchini. 

Kalonzo amedai kuwa kuna kikosi kinachoendeleza utekaji nyara huo na kupuuzilia mbali msimamo wa Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kuwa maafisa wa polisi hawahusiki katika utekaji nyara huo.

Isitoshe, amelalamikia hatua ya Kanja kutofika mahakamani kama alivyoagizwa na mahakama ili kuelezea waliko watu waliotekwa nyara katika siku za hivi karibuni.

Agizo la kumtaka Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI Mohamed Amin kufika mahakamani lilitolewa na Jaji Bahati Mwamuye Disemba 31, 2024.

“Kama upinzani, tunaamini kwa dhati kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Utekaji nyara huu lazima ukomeshwe,” alisema Kalonzo nje ya mahakama leo Jumatano akiwa ameandamana na viongozi wengine wa upinzani.

Mahakama imempa Kanja fursa ya mwisho kufika mahakamani ili kuelezea kilichowafanyikia vijana waliotekwa nyara la sivyo afungwe jela kwa kuidharau mahakama.

Kufikia sasa, ni watu watano pekee walioachiliwa: Ronny Kiplagat, Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli na Kelvin Muthoni.

Kijana mwingine, Steve Mbisi, bado hajulikani aliko.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *