Jimbo katoliki la Meru lapata askofu mpya

Askofu Jackson Murugara atachukua mahala pa askofu Salesious Mugambi atakapostaafu.

Marion Bosire and Jeff Mwangi
2 Min Read

Jimbo la Meru la kanisa katoliki limepata askofu mpya huku wakenya hasa waumini wa kanisa katoliki wakihimizwa wajiepushe na ufisadi.

Mwenyekiti wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB ambaye pia ni askofu wa jimbo la Kisumu Maurice Muhatia amesema ipo haja ya wakenya kutokomeza kabisa saratani ya ufisadi.

Muhatia alikuwa akizungumza katika uwanja wa michezo wa Kinoru katika hafla ya kusimika askofu wa dayosisi ya Meru Jackson Murugara atakayechukua mahala pa askofu Salesious Mugambi atakapostaafu.

Askofu huyo wa Kisumu alisema kwamba tangu jadi, kanisa limekuwa likitegemea michango ya waumini na wahisani wengine na hayo ndiyo maelekezo ya Yesu Kristo aliyeanzisha kanisa linaloaminiwa na wakristo wote.

Alisema hata hivyo kwamba kanisa katoliki halikubaliani na matoleo yanayotolewa kwa majivuno na katika jicho la umma ili kupata sifa hasa michango kutoka kwa wanasiasa.

Kulingana na askofu huyo mkuu, ni msimamo wa maaskofu wa kanisa katoliki kwamba michango inayotangazwa kwa namna hiyo huenda ikajumuisha pesa zilizopatikana kwa njia ya ufisadi ambao kanisa linalaani.

Alitoa wito kwa wakenya wakumbatie hulka njema na kukataa ufisadi ili nchi iwe yenye mafanikio.

Mwakilishi wa Papa Mtakatifu nchini Kenya na nchini Sudan Kusini Askofu mkuu Hubertus Van Megen alisema Kenya ni nchi ambayo inakabiliwa na tatizo la ufisadi.

Katika hotuba yake ya kwanza, askofu mpya wa dayosisi ya Meru inayojumuisha kaunti za Meru na Tharaka Nithi Jackson Murugara aliomba uungwaji mkono anapotekeleza majukumu yake mapya.

Alisema atashirikiana na mapadri wote na waumini wote wa dayosisi hiyo.

Website |  + posts
Share This Article