Jeshi la wanamaji kushirikiana na wadau kudumisha usafi baharini

Tom Mathinji
1 Min Read

Jeshi la wanamaji nchini limesema litashirikiana na jamii, mashirika na asasi za serikali kuhakikisha hakuna uchafuzi wa plastiki katika bahari, ulimwengu unapoadhimisha siku ya usafi wa maeneo ya Pwani.

Kwa mujibu wa shirika la umoja linalohusika na maswala ya mazingira –UNEP, kila mwaka takriban tani milioni 19 hadi 23 za taka za plastiki hutubwa katika bahari na kuhatarisha maisha ya viumbe vinavyoishi majini na mfumo mzima wa ekolojia.

Akizungumza katika hafla hiyo, iliyoandaliwa katika ufuo wa  Jomo Kenyatta kaunti ya Mombasa, naibu kamanda wa jeshi la wanamaji hapa nchini  Brigadier John Kiswa, alisema usafi huo ni muhimu kwa mazingira ya eneo hilo na afya kwa ujumla.

“Kila taka ambalo linatolewa, haliashirii tu usafi katika pwani, lakini pia kujitolea kwetu kudumisha mazingira bora kwa vizazi vijavyo,” alisema Kiswa.

Washiriki kutoka jamii ya eneo hilo, shule, mashirika ya serikali na asasi za serikali, walivumilia jua kali siku ya Jumapili kuzoa taka katika ufuo wa bahari.

Aidha alitoa  wito wa kufanywa kwa juhudi za pamoja katika kuhifadhi mazingira dhidi ya shughuli za binadamu na viwanda.

Aliwahimiza washiriki kutetea mazoea endelevu, kushinikiza  utatuzi bora wa usimamizi wa taka, na kushirikisha jamii katika mazungumzo yanayoendelea kuhusu utunzaji wa mazingira.

TAGGED:
Share This Article