Jeshi la ulinzi nchini Uganda kupitia kwa msemaji wake limetoa taarifa inayoelezea kuhusu ajali ya ndege ya jeshi la wanaanga katika eneo la Karamoja.
Taarifa hiyo ambayo imetiwa saini na Brigadia Mkuu Felix M. KUlayigye, inasema kwamba jana Jumamosi, Julai 29 saa kumi na dakika arobaini jioni, ndege ya jeshi la wanaanga wa nchi hiyo MI 24 nambari AF822 ilianguka katika kijiji cha Nadiket umbali wa kilomita 5.3 kutoka kambi ya jeshi ya Moroto.
Ndege hiyo ilikuwa inatekeleza operesheni ya kawaida wakati ajali ilitokea.
Rubani pamoja na wanajeshi wengine watatu ambao walikuwa kwenye ndege hiyo wanasemekana kuwa salama huku kundi la wataalamu kutoka kwenye jeshi la wanaanga likianzisha uchunguzi kufahamu kilichosababisha ajali hiyo.
Msemaji huyo wa majeshi ya ulinzi ya Uganda aliomba wananchi wa vijiji vilivyo karibu na eneo la tukio wasifike karibu nalo.