Jeshi la Sudan limechukua udhibiti kamili wa Ikulu ya Rais mjini Khartoum siku ya Ijumaa, Televisheni ya Sudan na vyanzo vya kijeshi vimesema.
Hii ni mojawapo ya mafanikio makubwa, katika mzozo wa miaka miwili unaotishia kusambaratisha nchi hiyo.
Jeshi lilikuwa likifanya msako katika maeneo yanayozunguka ikulu kuwasaka wanachama wa Kikosi cha RSF, duru zimesema.
Video na picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, zinaonyesha wanajeshi wakishangilia kwa bunduki zao na kupiga magoti kuomba.
Nabil Abdallah, msemaji wa jeshi, alisema kwenye Televisheni ya serikali kwamba wanajeshi walidhibiti ikulu na majengo ya wizara katikati mwa Khartoum.
“Vikosi vyetu viliharibu kabisa wapiganaji na vifaa vya adui, na kukamata vifaa na silaha nyingi,” Abdallah aliongeza.
Kundi la wapiganaji wa RSF kwa haraka lilichukua udhibiti wa ikulu na sehemu kubwa ya mji mkuu wakati wa kuzuka kwa vita mwezi Aprili 2023, lakini Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan katika miezi ya hivi karibuni vimerudi na kuelekea ikulu kando ya Mto Nile.
RSF, ambayo mapema mwaka huu ilianza kuanzisha serikali sambamba, inashikilia udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Khartoum na nchi jirani ya Omdurman, pamoja na magharibi mwa Sudan, ambako inapigania kutwaa ngome ya mwisho ya jeshi huko Darfur, al-Fashir.
Kuuteka mji mkuu kunaweza kuharakisha jeshi kuchukua kikamilifu Sudan ya kati, na kuimarisha mgawanyiko wa eneo la mashariki-magharibi kati ya nchi hizo mbili.
Pande zote mbili zimeapa kuendelea kupigania sehemu iliyobaki ya nchi, na hakuna juhudi zozote za mazungumzo ya amani zilizotekelezwa.
Vita hivyo vilizuka huku kukiwa na mzozo wa madaraka kati ya jeshi la Sudan na RSF kabla ya mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia.