Jennifer Lopez na Ben Affleck hatimaye wameafikia makubaliano ya ugavi wa mali katika mchakato wao wa talaka, miezi minne tangu Lopez kuwasilisha kesi ya kukomesha ndoa yao ya miaka miwili.
Hakuna yeyote kati ya wawili hao aliyeomba usaidizi wa kifedha kwa mwingine kulingana na makubaliano hayo.
Lopez alianzisha mchakato wa talaka Agosti mwaka jana na utengano wao ulijiri baada ya uvumi kusambaa kwamba walikuwa wanaishi maeneo tofauti.
Wakati huo Lopez alikatiza ziara yake ya kikazi na kwenda kukaa na familia yake kisha wakatangaza makazi yao ya Beverly Hills kwa mauzo.
Ndoa ya Lopez na Affleck ilijiri miaka 20 tangu wakati walikutana kwa mara ya kwanza katika maandalizi ya kipindi cha vichekesho cha ‘Gigli’ ambapo waliigiza kama wahalifu waliokuwa wakifanya kazi eneo moja na kuwa marafiki na hatimaye wapenzi.
Katika muda huo wa miaka 20, wote wawili waliingia kwenye ndoa na watu wengine na kuwa na familia kabla ya kuruduana mwaka 2021.
Novemba mwaka 2002 Ben alimvisha Lopez pete ya uchumba na wakapanga harusi Septemba 2003 lakini haikufanyika, sababu ikiwa kuangaziwa sana na vyombo vya habari.
Ilipofika Januari mwaka 2004 wakatangaza kwamba wameachana.