Rais William Ruto leo Jumamosi, amewaongoza wakenya kumwomboleza mkuu wa vikosi vya ulinzi marehemu Jenerali Francis Ogolla, aliyefariki Alhamisi kupitia ajali ya ndege katika kaunti ya Pokot Magharibi.
Huku akitaja uteuzi wa Jenerali Ogolla kuwa bora zaidi aliofanya akiwa Rais, Kiongozi wa taifa alimtaja Jenerali Ogolla kuwa afisa mjasiri, shupavu na aliyejitolea katika kazi yake.
“Jenerali Ogolla ambaye ni kamanda mwenye tajiriba, mwanahewa na mwanajeshi, alifariki alipokuwa akifanya kazi aliyoipenda zaidi, kuwaongoza maafisa wake kurejesha utulivu na amani katika sehemu iliyokumbwa na utovu wa usalama hapa nchini,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto alisema Jenerali Ogolla alidhihirisha kuwa alitoa kipaumbele kwa taifa hili na wananchi, na alitekeleza majukumu yake kwa uadilifu.
“Huwa hatupati fursa nyingi kutekeleza wajibu wetu. Hatujui wakati wa kuondoka kwetu hapa duniani. Tunaishi mara moja na tunapaswa kujitolea,” aliongeza kiongozi wa taifa.
Jenerali Ogolla ametajwa kuwa mchapakazi jasiri, mwenye maono na aliyeonyesha weledi wa hali ya juu alipotekeleza majukumu yake.
Atazikwa nyumbani kwake, kesho Jumapili nyumbani kwake Ng’iya, eneo bunge la Alego Usonga, kaunti ya Siaya