Jean Ojiro awakilisha Kenya kwenye Miss Universe

Tangu kuwasili Puerto Rico, Ojiro ameshiriki shughuli mbalimbali za kabla ya mashindano, akionyesha vazi lake liitwalo “The Wings of the Rift Valley”.

Marion Bosire
2 Min Read

Jean Ojiro kwa sasa anawakilisha Kenya kwenye mashindano urembo ya Miss Universe awamu ya 75, yanayofanyika huko San Juan, nchini Puerto Rico.

Hatua hii inaashiria kurejea kwa Kenya katika mashindano hayo ya kimataifa ya urembo.

Mwanamitindo huyo wa miaka 27, ambaye pia ni mtayarishaji wa maudhui ya kidijitali na mhitimu wa uandishi wa habari, alitwaa taji la Miss Universe Kenya 2026 mwezi Julai baada ya kushinda washiriki wapatao 1,000.

Safari ya Ojiro ilianza kwa kutuma maombi dakika za mwisho siku ya mwisho ya usajili na akakaribia kukosa mwaliko wa usaili baada ya ujumbe huo kuingia kwenye sehemu ya barua pepe taka.

Ushiriki wake pia unalenga kuhamasisha juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake nchini Kenya.

Tangu kuwasili Puerto Rico, Ojiro ameshiriki shughuli mbalimbali za kabla ya mashindano, akivutia watu kupitia kujiamini na namna anavyowakilisha utamaduni wa Kenya.

Alionyesha mavazi ya kitamaduni Novemba 21, 2026, vazi lake likipatiwa jina la “The Wings of the Rift Valley” yaani “Mabawa ya Bonde la Ufa”.

Jean Ojiro akionyesha vazi lake la The Wings of the Rift Valley

Vazi hilo la rangi ya waridi lililotokana na ndege aina ya flamingo wanaopatikana Ziwa Nakuru na maziwa mengine ya Bonde la Ufa, liliwakilisha urithi wa asili wa Kenya na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.

Ojiro atachuana na warembo wengine 115 kuwania taji la Miss Universe katika Ukumbi wa José Miguel Agrelot Coliseum kwenye fainali Novemba 24, 2026.

Share This Article