Kituo cha jeshi la wanaanga cha Wajir, kilibuniwa Februari 25, 1974, jukumu lake kuu likiwa ni kulinda anga za taifa hili dhidi ya maadui.
Ili kuhakikisha kikosi hicho kinatekeleza majukumu yake ipasavyo, kikosi hicho kilipokea na kukamilisha mafunzo kabambe kuhusu utumizi wa zana za kisasa za kivita.
Kituo hicho almaarufu “Wajir Air Base”, ambacho sasa kinaongozwa na Brigedia Stephen Kerempe, kilijukumiwa kulinda maeneo muhimu hapa nchini, kuambatana na taratibu za majukumu ya jeshi la wanahewa (KAF).
Tangu kubuniwa kwake, kituo hicho kimenakili ufanisi mkubwa katika shughuli zake ambazo zinajumuisha kuopoa miili ya waahiriwa wa ajali katika mto Enziu mwezi Disemba mwaka 2021.
Wanajeshi hao pia walihusika katika kuwaokoa zaidi ya wakazi 200, walioathiriwa na maporomoko ya ardhi Pokot Magharibi mwaka 2019 kufuatia mvua kubwa.
Wakati huo huo kituo hicho cha wanajeshi wa angani cha Wajir, kilitekeleza jukumu kubwa la kuwaokoa wakazi na mali yao waliosombwa na mafuriko katika kaunti ya Baringo mnamo Mei 1, 2020.
Rais William Ruto leo Alhamisi alikabidhi kituo hicho bendera ya taifa na ikle ya fahari, ishara kwamba sasa kinaweza kujisimamia katika shughuli mbali mbali, bila kutegemea makao makuu ya kikosi cha wanajeshi wa angani (KAF).
Kituo hicho kilipokea bendera hizo wakati wa maadhimisho ya sherehe za 61 za Jamhuri katika uwanja wa Uhuru Gardens Jijini Nairobi.