Jamii za Murule na Degodia zimeafikia mapatano muhimu ya amani baada ya siku nne za mazungumzo.
Wazee, viongozi wa kidini na wawakilishi wa eneo hilo walishiriki mazungumzo hayo na kuafikia mapatano ambayo yanatizamiwa kusuluhisha mizozo ya muda mrefu.
Maeneo ya Sala, Lafey na Rhamu katika eneo bunge la Mandera Kaskazini yamekuwa yakishuhudia migogoro kati ya jamii hizo kwa miaka mingi.
Katika siku za hivi karibuni, migogoro hiyo ilisababisha uharibifu wa mali na shule kufungwa.
Mkataba wa amani ulioafikiwa umeorodhesha hatua kadhaa ambazo lazima zichukuliwe mara moja kama vile kusitisha mapigano, kuvunjwa kwa makundi ya wapiganaji, kutolewa kwa huduma za ulinzi kwa wanaosafiri, kuimarisha upatikanaji wa maji na kuondolewa kwa vikwazo vyote vya watu kuzoa kuni na kulisha mifugo.
Mapatano hayo kadhalika yanaelekeza kwamba kamati ibuniwe ya kuhakikisha utekelezaji wa mipango yote ya maridhiano na kushughulikia changamoto ibuka.
Kundi la kukadiria uharibifu pia litabuniwa na wazee wa jamii hizo ambazo zimekubali kuwasilisha mizozo ya ardhi ili itatuliwe.
Gavana Mohamed Khalif wa kaunti ya Mandera aliyeongoza mkutano huo wa kutafuta amani alitaka amani idumu, shule zifunguliwe na wakazi wajitolee kikamilifu kwa maridhiano.
Wabunge Bashir Abdullahi wa eneo la Mandera Kaskazini na Mohamed Abdiker wa Lafey wanahimiza wadau wote wa mapatano hayo washughulikie vyanzo vya migogoro na kuomba maafisa wa usalama wachukue hatua kali dhidi ya wanaotaka kuvuruga mipango ya kutafuta amani.
Mapatano hayo kati ya jamii za Degodia na Murule yanaleta matumaini ya kuafikiwa kwa amani ya kudumu katika kaunti ya Mandera.