Jamii yaombwa kukumbatia wafungwa wa zamani

Marion Bosire
2 Min Read

Mratibu wa majaribio wa kaunti ya Laikipia Francis Kamau amehimiza familia mbalimbali na jamii kwa ujumla kukumbatia wafungwa wa zamani.

Akizungumza kwa vyombo vya habari mjini Nanyuki katika hafla ya wiki hii ya ukumbusho wa huduma za urekebishaji yenye kauli “afya ya ubongo”, Francis alifichua kuwa, wafungwa wa zamani wanakumbana na ubagusi katika jamii licha ya kuwa na ujuzi wa kazi mbalimbali kama vile uashi, ususi na ushona nguo waliojifunza gerezani na ambao wanaweza tumia kujimudu na kuinua jamii.

“Wanapotoka gerezani huwa wamerekebika, hivyo tunaomba familia zetu na jamii kuwakubali tena. Musiwaone kama wavunja sheria tena kwa sababu wamefunzwa ujuzi mbali mbali. Wakiwa nje ya gereza wanaweza jitegemea wenyewe”, Alisema Kamau.

Naye msimamizi wa magereza katika gereza la Nanyuki – Danson Atama, alitaja kuwa huwasaidia wafungwa kupitia mafunzo ya dini na ujuzi mbalimbali wanapohudumia vifungo vyao.

Kwenye kauli mbiu, Atama alihoji kuwa, “Tunajaribu kuhakikisha afya ya akili kwa lengo la huduma bora katika sehemu za kazi. Tunawarekebisha kwa haki na kuwasaidia kushinda msongo wa mawazo kwa njia mbali mbali kama vile michezo”, Alihoji Atama.

Katika hafla hiyo, waratibu wa majaribio walipewa mafunzo ya kushughulikia maswala ya msongo wa mawazo kama vile mkazo wa kihisia, mabadiliko ya kiakili,uchovu wa huruma na waliookoka na uhusiano wa kimawazo baina yao na wafungwa kwa shabaha ya huduma bora.

Siku ya ukumbusho ya urekebishaji katika magereza huadhimishwa tarehe 22 ya mwezi wa Oktoba kila mwaka.

Share This Article