Jamii ya Maa yapongezwa kwa kudumisha utamaduni

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais William Ruto ameipongeza jamii ya wamaasai kwa kujitolea kudumisha utamaduni wao pamoja na mazingira.

Akiongea Jumanne alipofungua rasmi tamasha la kitamaduni la jamii ya wamaasai eneo la Maasai Mara, katika kaunti ya Narok, rais alisema serikali kuanzia sasa itaunga mkono tamasha hilo kila mwaka, na vile vile kuboresha usimamizi wa mbuga za kitaifa ili kuhakikisha matumizi endelevu na kwa manufaa ya kaunti husika.

Aidha alisema wizara ya utalii itashirikiana kwa karibu na jamii hiyo na kukuza utamaduni wao ili kuleta mapato kupitia utalii.

Kiongozi wa taifa pia aliahidi kwamba jamii zote ambazo zimetoa ardhi yao ya kulisha mifugo kutumika kwa shughuli za uhifadhi wanyama pori, kwamba sasa watanufaika moja kwa moja kupitia sera mpya.

Alisema serikali imeanza kugawa mapato kutoka mbuga za wanyama pori kwa usawa na kaunti husika.

Vile vile alisema mipango inaendelea kuhakikisha usimamizi wa mbuga ya kitaifa ya Amboseli umekabidhiwa serikali ya kaunti ya Kajiado.

Share This Article