Katika eneo la Gitimbene karibu na mji wa Meru tunakutana na jamaa kwa jina Zakaria Wanyaga. Zakaria ambaye alisomea ufundi wa stima kwenye magari katika mojawapo ya vyuo anwai vya kaunti ya Meru, amekuwa akifanya kazi hiyo kwa miaka mitatu sasa kwenye karakana moja ya Gitimbene.
Kilichotushangaza na kufanya atambulike sio weledi wake katika kurekebisha nyaya za stima kwenye gari bali ni uvumbuzi wake wa kipekee ambapo ametumia vyuma kuu kuu kutengeneza baisikeli ambayo inatumia injini ya pikipiki.
Zakaria, anasema alifikiria kutengeneza baisikeli ya aina hiyo baada ya kuona bei ya pikipiki ikipanda kila kuchao.
Baisikeli hiyo ambayo ina taa za ishara, bomba na betri inatumika tu kama pikipiki lakini inatumia mafuta kidogo ikilinganishwa na pikipiki.
Anasema kuunda baiskeli hiyo haikuwa rahisi lakini alisukumwa na mapenzi yake kwa uvumbuzi ndiposa akakamilisha mradi huo.
Zakaria sasa anashauri vijana kuangazia talanta zao na watafanikiwa maishani na kamwe wasiache kutia bidii katika kuboresha na kuimarisha talanta hizo.
Tumaini lake sasa ni kwamba serikali itaidhinisha uvumbuzi wake na kumsaidia kifedha ili aweze kuunda baisikeli nyingi kama hizo ili kunufaisha wale ambao wangependelea kuwa nazo.
Alisema injini inagharimu shilingi elfu 30.
Zakaria anasema pia kwamba baisikeli yake inatunza mazingira kwani haitumii mafuta mengi na hivyo kupunguza gesi itokanayo na mafuta ambayo huchangia katika uchafuzi wa mazingira.