Jamaa aokolewa siku 8 baada ya matetemeko Venezuela

Waokoaji walimgundua siku tatu zilizotangulia kuokolewa kwake jana.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamume ameokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka siku nane baada ya matetemeko mawili makubwa ya ardhi kutokea nchini Venezuela.

Uokoaji huo ulifanyika Alhamisi wakati juhudi zilibadilishwa kutoka kutafuta manusura chini ya vifusi na kuelekezwa katika kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya maelfu ya wakazi waliopoteza makazi yao.

Inakadiriwa kuwa majengo elfu 60, yaliharibiwa katika mitetemeko ya ardhi ya wiki iliyopita, iliyokuwa na ukubwa wa kipimo cha 7.2 na 7.5 mtawalia, huku watu 13,000 wakiachwa bila makazi.

Katika taarifa yake ya mwisho rasmi, serikali ya Venezuela ilisema kuwa watu wasiopungua 2,295 wamethibitishwa kufariki, huku 11,000 wakijeruhiwa. Idadi ya vifo ilitarajiwa kuongezeka, huku takriban watu 50,000 wakiripotiwa kupotea.

Hata hivyo, katika mwanga wa nadra wa matumaini, waokoaji waliweza kumfikia mlinzi wa umri wa miaka 43, Hernan Gil, Alhamisi, baada ya siku kadhaa za kujaribu kumtoa.

Alikuwa amekwama kwenye jengo la ghorofa saba lililoporomoka ambako alikuwa akifanya kazi katika eneo la pwani la Catia La Mar lililoathirika vibaya.

Gil alipatikana siku tatu zilizopita ambapo makundi ya uokoaji kutoka nchi saba, zikiwemo Venezuela, Chile, Marekani, Ureno, Costa Rica, El Salvador na Mexico, yalifanya kazi kwa pamoja ili kumwokoa.

“Huu ni muujiza wa kweli,” mke wa Gil, Gusbimar Gonzalez, aliliambia shirika la habari la AFP.

Cristian Vera, kiongozi wa kundi la uokoaji kutoka Chile, aliiambia wanahabari kwamba waokoaji hatimaye waliweza kuchimba handaki lenye urefu wa mita tatu ili kumtoa Gil.

Kabla ya kufanikiwa kumwokoa, wahudumu hao walikuwa wakimpelekea maji kupitia bomba na kumpatia hewa ya oksijeni kwa kutumia mpira maalumu.

“Haikuwa rahisi kufika mahali mwathirika alikuwa,” alisema Vera.

Huku kuokolewa kwa Gil kukizipa baadhi ya familia matumaini, juhudi nyingi za uokoaji kote nchini humo zimeishia kwa huzuni.

Wanaotoa misaada ya kibinadamu wameonya kwamba athari za mitetemeko hiyo huenda zikasababisha mgogoro wa afya, kwani vituo vya matibabu vyenye uhaba wa wafanyakazi vinaweza kukabiliwa na majeraha yasiyotibika na magonjwa ya kuambukiza.

Share This Article