Jamaa kwa jina Ramadhani Shaban wa umri wa miaka 21 amekamatwa na maafisa wa polisi wa mkoa wa Kigoma kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kuhusu kutekwa nyara.
Ilibainika kwamba Shaban ambaye anajulikana sana kama Kocha na ambaye anaishi Buronge Manispaa ya Kigoma Ujiji alijiteka nyara akisaidiwa na marafiki.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amesema kwamba Shaban alitekeleza kosa hilo Mei 14, 2024 na alidai shilingi milioni 2.5 kutoka kwa wazazi wake kama fidia.
Akiwa mafichoni alipiga simu kwa wazazi wake na kuwataka watoe fedha hizo ndiposa aachiliwe na kwamba wakichelewa kutoa atauawa.
Wazazi wake aliamua kutoa taarifa kwa polisi wakiamini mwanao ametekwa nyara na uchunguzi ukaanzishwa huku polisi wakiwashauri wasitume pesa zozote.
Polisi wakiendeleza uchunguzi, wazazi wake walifika kwenye kituo cha polisi wakiwa naye na kueleza kwamba amepatikana leo katika eneo la Msimba Dampo nje kidogo ya Manispaa ya Kigoma Ujiji baada ya kutoa fedha kwa Watekaji.
Hata hivyo polisi waligundua kwamba mtuhumiwa na marafiki zake wawili Kassim Kibona na Ramadhani Issa walitoa taarifa za uongo ili kupata pesa.
Wote watatu walikamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani punde uchunguzi utakapokamilika.