Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga alaani visa vya utekaji nyara

Martin Mwanje
4 Min Read
David Maraga - Jaji Mkuu Mstaafu

Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga amelaani vikali visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara nchini akivitaja kuwa ukiukaji wa katiba na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kuvikomesha. 

Maraga ametaka vijana wote ambao wametekwa nyara kuachiliwa huru mara moja.

“Nalaani mauaji, mateso na visa vya utekaji nyara na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa vijana ambao bado wanashikiliwa kinyume cha sheria,” amesema Maraga kwenye taarifa yake ya kuwatakia Wakenya heri ya Mwaka Mpya.

“Siasa zetu kamwe hazipaswi tena kufikia kiwango hiki cha ukatili na kutojali.”

Maraga ametaka wote waliowasababishia Wakenya makovu yasiyoelezeka mwaka huu kuwajibishwa katika Mwaka Mpya wa 2025.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR imesema visa 13 vya utekaji nyara vimeripotiwa nchini katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

KNCHR inasema hii inafanya jumla ya visa vilivyoripotiwa tangu mwezi Juni mwaka huu kufikia 82.

Kulingana na KNCHR, visa 7 vya utekaji nyara vilirpotiwa mwezi huu wa Disemba huku watu 6 wakiwa bado hawajulikani waliko.

Visa hivyo viliripotiwa katika kaunti za Machakos, Embu, visa 4 katika kaunti ya Nairobi ingawa mtu mmoja aliyekuwa ametoweka katika eneo la Ruaraka amepatikana huku kisa kimoja kikiripotiwa katika kaunti ya Kiambu.

Idadi ya jumla ya watu ambao bado hawajulikani waliko tangu mwezi Juni mwaka huu sasa imefikia 29.

KNCHR, kupitia mwenyekiti wake Roseline Odede, aimelalamikia hatua ya maafisa wa polisi kushindwa kuwakamata wahusika wa visa hivyo ambavyo anasema vinafanyika peupe wakati wa mchana na baadhi ya wahusika kunaswa kwenye kamera za usalama.

Idara ya Mahakama pia imelaani visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara humu nchini.

Kwenye taarifa, idara hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome imelaani kuchipuka tena kwa visa vya utekaji nyara ikivitaja kuwa ukiukaji wa sheria.

“Idara ya Mahakama imepata kufahamu ripoti za hivi karibuni za kuibuka tena kwa visa vya utekaji nyara. Kenya ni nchi ya kidemokrasia inayoongozwa na katiba, ambapo utawala wa sheria unasimama kama maadili ya msingi na kanuni elekezi ya maongozi yetu,” imesema idara hiyo.

“Utekaji nyara hauna nafasi katika sheria na ni tishio la moja kwa moja kwa haki za raia.”

Kufuatia kuibuka kwa ripoti hizo, Idara ya Mahakama inatoa wito kwa asasi za usalama na taasisi husika kutii sheria ili kulinda haki na uhuru wa raia.

Kwa upande wake, Huduma ya Taifa ya Polisi nchini, NPS imekanusha madai kwamba maafisa wa polisi wanahusika katika visa vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini kwa sasa.

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja ameelezea kutoridhishwa na taarifa zinazosambazwa zikiwatuhumu maafisa wa polisi kwa utekaji nyara huo akizitaja kuwa za uongo.

Kanja anasema mamlaka ya maafisa wa polisi yanahusu tu kuwakamata wanaovunja sheria kwa njia inayokubalika na wala sio kuwateka nyara.

“Mchakato kulingana na sheria za huduma uko wazi: shughuli zote za kukamata wahalifu lazima zinakiliwe kwenye kitabu cha matukio ili wafikishwe mahakamani baadaye,” alielezea Kanja awali kwenye taarifa yake.

Amesema iwapo mtu hatafikishwa mahakamani basi anafaa kuachiliwa huru.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *