Majaji wa kusikiliza kesi ya kupinga sheria ya fedha wateuliwa

Marion Bosire
2 Min Read

Jaji Mkuu Martha Koome ameteua jopo la majaji watatu litakalosikiliza na kuamua kesi ya kupinga sheria ya fedha ya mwaka 2023.

Jaji David Majanja ataongoza jopo hilo akisaidiwa na majaji Lawrence Mugambi na Christine Meoli. Jopo hilo sasa linatarajiwa kutangaza tarehe ya kusikiliza kesi hiyo.

Awali, Jaji wa Mahakama Kuu Mugure Thande alitoa agizo la kusimamisha utekelezwaji wa sheria hiyo ya fedha. Amekuwa akiongeza muda wa kusimamisha utekelezaji huo hadi kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah na wengine isikilizwe na kuamuliwa.

Katika kikao cha mwisho, Jaji Mugure aliamua kwamba faili ya kesi hiyo ipelekwe kwa Jaji Mkuu ili ateue jopo la majaji ambalo litasikiliza na kuamua kesi hiyo. Alisema sheria hiyo inaathiri umma na angeondoa agizo la kusimamisha utekelezaji wake basi Wakenya wangeumia.

Serikali kupitia mawakili wake wakiongozwa na Profesa Githu Muigai, ilitaka agizo hilo la mahakama kuu litupiliwe mbali kwani linakwamisha mipango ya serikali.

Kuhusu shtaka jingine lililoongezwa dhidi ya mamlaka ya kudhibiti bei ya mafuta nchini, EPRA kwa kuongeza bei ya mafuta hata baada ya mahakama kuagiza kusitishwa kwa utekelezaji wa sheria ya fedha, mawakili wa serikali walisema iwapo mahakama ingependelea walalamishi kwenye uamuzi, itakuwa vigumu kwa serikali kurudisha mapato ambayo imejipatia kutokana na ongezeko la ushuru ziada wa thamani, VAT kwa bidhaa za petroli na mafuta.

Ushuru huo awali ulikuwa wa kiwango cha asilimia 8 na sheria ya fedha ya mwaka huu ikauongeza hadi asilimia 16.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *