Jaji mkuu Martha Koome anataka hatua za haraka zichukuliwe kuhusiana na ripoti iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa polisi iliyosema kwamba wanawake 97 wameuawa katika muda wa siku 90.
Koome amesema mauaji hayo sio tu jinai bali pia ni vitendo vya kinyama na familia za waathiriwa zinapaswa kupata usaidizi kwani zinapitia wakati mgumu.
Alikuwa akizungumza katika kituo cha kurekebisha mienendo cha wasichana cha Kirigiti alipozindua maadhimisho ya kitaifa ya mwezi wa haki za watoto mwaka 2024.
Jaji mkuu aliyekuwa ameandamana na maafisa wengine wakuu wa idara ya mahakama aliomba watekelezaji sheria, wanaharakati na makundi mengine kuchukua hatua kuhakikisha unyama huo unakomeshwa.
Mada ya mwaka huu ya mwezi wa haki za watoto ni, “Kuimarisha Haki za watoto kupitia Uchunguzi wa Awali : Kukuza Urekebishaji, Kuunganishwa tena na Utu kwa Watoto Walio katika Migogoro na Sheria.”
Koome alisema mada hiyo inahimiza kukumbatia suluhisho zinazoangazia mahitaji ya kipekee ya kila mtoto, sio kama wakosaji lakini kama vijana wanaohitaji kueleweka, kuhurumiwa na kuelekezwa.
“Katiba pamoja na sheria ya watoto ya mwaka 2022, zimeainisha haki za kila mtoto kutunzwa, kulindwa na kurekebishwa.” alisema jaji mkuu akisema watoto wakosaji mara nyingi huwa wamekumbwa na changamoto zinazowazidi.
Kutokana na hilo, Koome alisema hawafai kuangaziwa tu kama kesi bali wanafaa kuchukuliwa kama watoto wanaohitaji usaidizi wa wote na wa kuingilia kati.
Koome anahimiza ushirikiano wa karibu kati ya madaktari na wataalamu wa masuala ya akili ili kuweza kusaidia watoto hao, kuwarekebisha na kuwaunganisha tena na jamii kwa ufanisi.
“Kama jaji mkuu na mwenyekiti wa baraza la kitaifa la utekelezaji haki, ninaahidi kuhakikisha usaidizi wa masuala ya kiakili na ushauri nasaha mahakamani pamoja nanyi ili ili kuunda sera za kutoa usaidizi huo kwa watumizi wa mahakama na maafisa wa idara ya mahakama.” alisema Koome.
Jaji Teresa Matheka aliyehutubia mkutano huo alisema kwamba kuna kesi 9,900 za watoto katika mahakama mbali mbali kote nchini.
Matheka hata hivyo alisema kwamba kesi hizo ambazo zinahusu watoto moja kwa moja na nyingine zisizo za moja kwa moja zinashughulikiwa kila siku ili kuzipunguza.