Jaji Mkuu Martha Koome amejitolea kutetea utunzanji wa mazingira katika sekta ya haki nchini kupitia kuhakikisha sheria inafuatwa, kulinda haki, kuhakikisha maendeleo enedelevu na kutetea uendelevu wa ikolojia.
Koome aliyezungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo elekezi wa kimkakati wa mfumo wa haki wa kutunza mazingira alisema ari ya kutafuta haki inawiana na uendelevu wa mazingira na sekta ya haki inafaa kuongoza kwa matendo na kuwa mfano wa kuigwa na sekta nyingine.
Alitambua kwamba awali, mfumo wa haki haukuzingatia athari za mipango yake kwa mazingira na hivyo uendelevu huo ni lazima uangaziwe upya kwa kujitolea kuleta mabadiliko na ushirikiano wa utoaji bora wa haki.
Jaji Koome alisema pia kwamba mfumo uliozinduliwa unataka mashirika mbali mbali ya sekta ya haki kuwianisha mipango ya utunzanji wa mazingira kwenye mipango yao ya kila siku.
Alijitolea kutekeleza mabadiliko katika upatikanaji wa haki ambayo yatapiga jeki haki za kimazingira ili kuhakikisha sheria na mipango ya kisheria vinapigia debe uendelevu wa mazingira.
“Huko mashinani tutaongeza mipango ya utunzaji mazingira kupitia kamati za watumizi wa mahakama ili kuleta mipango ya utunzaji mazingira karibu na jamii tunazohudumi,” alisema Koome.
Mfumo elekezi wa kimkakati uliozinduliwa unawataka pia wahusika wa sekta ya haki kutekeleza mabadiliko na kuingilia kati ili kuboresha utoaji na upatikanaji wa haki kwa watu waliotelekezwa hasa wanaoathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya tabia nchi.