Sera ya ‘kesi kutoahirishwa’ kutumiwa kuepusha ukawiaji wa kesi

Martin Mwanje
2 Min Read

Idara ya mahakama imeazimia kuanzisha “sera ya kesi kutoahirishwa” ili kuepukana na ucheleweshaji wa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi. 

Idara hiyo siku zilizopita imelaumiwa kwa kukawia kusikiliza na kuamua baadhi ya kesi ambazo wakati mwingine huchukua hata zaidi ya mwongo mmoja kabla ya hukumu kutolewa.

Hali hiyo imetajwa kuwa mojawapo ya sababu zinazochangia mrundiko wa kesi nchini.

Hata hivyo mambo huenda yakabadilika, ikiwa azimio lililochukuliwa na wakuu wa mahakama wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome litazingatiwa.

“Ili kuhakikisha utendakazi bora na kukabiliana na tatizo la ukawiaji katika kumaliza kesi zinazosikilizwa, mahakama za juu zitatekeleza sera ya “kesi kutoahirishwa”. Watumiaji wa mahakama na wadau wengine katika sekta ya haki wanaombwa kukumbatia sera ya “kesi kutoahirishwa” kwani uahirishaji kesi utakubaliwa tu katika hali zisizokuwa za kawaida,” ilisema taarifa kutoka kwa wakuu wa mahakama baada ya kukamilika kwa mkutano wao wa ushauriano.

“Tunatoa wito kwa wadau katika sekta ya haki kuunga mkono na kufanya kazi na idara ya mahakama katika kuboresha juhudi zinazolenga kuhakikisha kesi zinaamuliwa haraka.”

Katika taarifa hiyo, Jaji Koome alisema mahakama zitaimarisha mfumo wa usimamizi wa kesi ili kuboresha usimamizi wa kesi hizo.

Wakuu wa mahakama pia wameazimia kukabiliana vilivyo na zimwi la ufisadi ambalo limedaiwa kuizonga idara ya mahakama.

Na huku wakitambua matishio ambayo idara hiyo imekumbana nayo yakiwemo mashambulizi dhidi ya majaji na maafisa wa mahakama na kutoheshimiwa kwa maagizo ya mahakama, Wakenya wametakiwa kuendelea kuunga mkono uhuru wa idara ya mahakama.

Share This Article