Jaji aagiza kuharibiwa kwa stakabadhi zilizotwaliwa kutoka kwa seli ya Diddy

Marion Bosire
1 Min Read

Jaji anayeshughulikia kesi ya mwanamuziki wa Marekani P Diddy ameagiza kuharibiwa kwa stakabadhi zilizotwaliwa kutoka kwa seli yake.

Uamuzi huo ulitolewa katika kikao cha dharura Jumanne Novemba 19, 2024 kufuatia ombi la mawakili wa Diddy.

Wakili Marc Agnifilo alikuwa amelaumu maafisa wa mashtaka kwa kufikia stakabadhi za siri kupitia msako waliotekeleza kinyume cha sheria kwenye seli ya mteja wake na kutaka kuzitumia dhidi yake.

Maafisa hao wa upande wa mashtaka walikana madai ya kupata kurasa 19 za maandishi ya Diddy lakini jaji Arun Subramanian alimuunga mkono Diddy na wakili wake akitaka nakala zote za maandishi hayo ziharibiwe.

Waendesha mashtaka walidai kwamba Diddy alikuwa anajaribu kushawishi mashahidi na waamuzi wa kesi yake kupitia mawasiliano ya pande tatu.

Walidai pia kwamba alikuwa anaongoza wanawe kuandka kwenye mitandao ya kijamii maneno ya kumpendelea.

Mawakili wanaomtetea Diddy walisema hawakufahamishwa kuhusu msako wa seli yake kabla ya kuutekeleza na hivyo haki za mteja wao zilikiukwa.

Jaji Subramanian alifafanua kwamba waendesha mashtaka hawafai kutumia habari zozote kutoka kwa maandishi hayo ya Diddy hadi atakapoamua iwapo yatahusishwa kwenye kesi kama ushahidi.

Kesi hiyo imepangiwa kusikilizwa Mei 5, 2025.

Share This Article