Jada Pinkett akashifiwa kwa kuwa mbinafsi

Marion Bosire
2 Min Read

Jada Pinkett Smith amekashifiwa na wengi mitandaoni kwa kile wanachokitaja kuwa ubinafsi na kutumia jina la mume wake Will Smith kujiendeleza.

Jada wa umri wa miaka 52 alijipata matatani baada ya kufichua kwenye mahojiano kwamba yeye na Will wa umri wa miaka 55, walitengana yapata miaka 7 iliyopita japo hawajatalikiana.

Mahojiano hayo yalilenga kutangaza kitabu chake kijacho kwa jina “Worthy”.

Sasa wafuasi wa familia hiyo maarufu mitandaoni wamemgeukia Jada wakimtaja kuwa mnafiki na mbinafsi kwa kumkana Will ambaye ameonekana kutetea na kulinda ndoa yao.

Wengi wanashangaa ni kwa nini Will alihatarisha kazi yake alipomtetea Jada kwa dhati kwa kumzaba kofi mchekeshaji Chris Rock kwenye hafla ya tuzo za Oscar, Machi 27, 2022, iwapo walitengana mwaka 2016.

Rock ambaye alikuwa jukwaani kutuza mshindi, alitania upara wa Jada ambao unasababishwa na tatizo la kiafya kwa jina “Alopecia”.

Hatua ya Will Smith ilisababisha adhabu kali dhidi yake kama vile kususiwa na watayarishaji filamu wa Hollywood na kupigwa marufuku kwenye tuzo za Oscar kwa muda wa miaka 10.

Jada amekuwa akimwaga mtama kuhusu matatizo ya ndoa yake ambapo awali alisema aliwahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki August Alsina, uhusiano ulioanza mwaka 2016, akiwa bado kwenye ndoa na Will Smith.

Smith alitiririkwa na machozi walipojadili suala hilo kwenye kipindi cha Jada almaarufu “Red Table Talk”.

Share This Article