Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya shambulio la Israel dhidi ya Rafah, mji wa kusini kabisa wa Gaza, huenda likasababisha “mauaji”.
Mkuu wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths amesema Wapalestina mjini Gaza, tayari wanateseka kutokana na “mashambulizi makubwa yasiyo na mfano, na ukatili mkubwa”.
Matokeo ya uvamizi wa Rafah yatakuwa “janga”, alisema.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwashinda wapiganaji wa Hamas anaosema wamejificha katika mji huo.
Katika taarifa yake yenye maneno makali , Bw Griffiths alisema zaidi ya watu milioni moja “wamejazana mjini Rafah, wakitazama kifo usoni”. Alisema raia katika jiji hilo wana chakula kidogo na upatikanaji wa dawa ni wa kiwango cha chini na “hakuna mahali salama pa kwenda”.
Aliongeza kuwa uvamizi wa Israeli katika mji huo, “utaacha operesheni dhaifu ya kibinadamu kwenye mlango wa kifo”.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikiambia kipindi cha BBC cha Newshour kuwa Umoja wa Mataifa ghautapokea mpango wowote wa kuwahamisha wa Rafah kutoka kwa Israel na hautashiriki katika uhamishaji wowote wa lazima.
Stephane Dujarric alisema: “Umoja wa Mataifa hautakuwa sehemu ya kuwalazimisha watu kuhama.”