Israel yalaumiwa kwa kusababisha uharibifu mkubwa Jenin

Marion Bosire
2 Min Read

Umoja wa Mataifa umeilaumu Israel kwa kusababisha uharibifu wa kiwango cha juu katika kambi ya wakimbizi ya Jenin huko West Bank ambapo wanajeshi wa Israel wanaendeleza mashambulizi.

Madhambulizi hayo yamesababisha wakazi wa eneo hilo wmbao ni wapalestina bila chakula, maji, umeme na hata huduma za mtandao.

Wahudumu wa afya wa Kipalestina wanasema hatua ya kusitisha vita kikweli inahitajika katika eneo la Gaza kutoa fursa kwa kampeni ya kutoa chanjo ya polio.

Mashambulizi ya Israel katika eneo hilo yamesababisha vifo vya watu 61 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Raia wa Israel waliandamana kwa mara nyingine mjini Tel Aviv wakimtaka waziri mkuu Benjamin Netanyahu akubali kusitisha vita mara moja na Hamas ili kuruhusu kuachiliwa kwa mateka walioko Gaza.

Tangu Oktoba 7 mwaka jana, watu elfu 40,691 wameuawa katika ukanda wa Gaza huku elfu 94,060 wakiachwa na majeraha. Israel inalipiza kisasi shambulizi la Hamas nchini humo siku hiyo ambapo watu 1,139 raia wa Israel waliuawa.

Naibu mkurugenzi wa utayari wa majanga katika shirika la HOPE Chessa Latifi, anasema vita, kupoteza makazi na kuharibika kwa mfumo wa huduma za afya katika ukanda wa Gaza huenda vikaifanya iwe vigumu kutoa chanjo ya Polio.

Akizungumza huko Los Angelesnchini Marekani, Latifi alisema hakuna hakikisho la usalama kwa watakaoleta wanao kliniki kupokea chanjo hiyo na hata hawana namna ya kufika kwenye kliniki.

Latifi alisema pia kwamba chanjo hiyo pekee hata hivyo haitakomesha kusambaa kwa virusi kwani visababishi ni uchafu na ukosefu wa maji safi.

Mifumo ya usafi kama mifereji ya maji safi, vyoo na bafu katika ukanda wa Gaza imeharibiwa katika mashambulizi ya Israel kulingana na Latifi.

Share This Article