Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limetoa taarifa likisema Kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar aliuawa na wanajeshi wake katika operesheni iliyofanyika kusini mwa Gaza jana baada ya “kuwindwa kwa mwaka mzima”.
Haya yanajiri baada ya waziri wa mambo ya nje wa Israel Israel Katz kuwaambia viongozi wenzake kote duniani kuwa Sinwar aliuawa leo. Sababu ya kutofautiana kuhusu siku ya kuuwa kwake haijulikani wazi.
Katika taarifa, IDF inasema Sinwar alipanga na kutekeleza shambulio la Oktoba 7 na “alihusika na mauaji na utekaji nyara wa Waisraeli wengi”.
“Yahya Sinwar aliondolewa baada ya kujificha kwa mwaka uliopita nyuma ya raia wa Gaza, juu na chini ya ardhi katika mahandaki ya Hamas katika Ukanda wa Gaza,” inasema.
Jeshi la Israel linasema limekuwa likiendesha shughuli zake kusini mwa Gaza kufuatia taarifa za kijasusi “zilizoonyesha maeneo yanayoshukiwa ya wanachama wakuu wa Hamas”.
Wanajeshi wa IDF kutoka Brigedi ya 828 inayofanya kazi katika eneo hilo “waliwatambua na kuwaondoa magaidi watatu”, inasema, na kuongeza mchakato wa kuwatambua mmoja wa waliouawa alikuwa Sinwar.