Israel yaapa kuweka mbele ‘maslahi ya taifa’ katika kujibu shambulizi la Iran

Martin Mwanje
2 Min Read

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo Jumanne imesema kuwa Israel — na wala siyo Marekani — itaamua namna itafanya shambulizi la kulipiza kisasi baada ya Iran kurusha takriban makombora 200 katika nchi yake mapema mwezi huu. 

Matamshi hayo yanakuja wakati kamanda wa ngazi za juu wa Iran, ambaye kutokuwepo kwake kuliibua uvumi kuwa huenda aliuawa katika shambulizi la Israel, alionekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha wiki kadhaa.

Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran pia zilifyatuliana risasi wakati mapigano yakirindima nchini Lebanon huku makundi ya kutoa misaada yakionya juu ya hali mbaya ya kinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Oktoba mosi mwaka jana, Iran ilirusha msururu wa makombora yapatayo 200 nchini Israel kufuatia shambulizi la Israel katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Shambulizi hilo lilimuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah na jenerali wa Iran Abbas Nilforoushan.

Israel imeapa kulipiza kisasi shambulizi hilo. Rais wa Marekani Joe Biden — ambaye serikali yake ni msambazaji nambari moja wa silaha wa Israel — ameonya dhidi ya kushambulia vituo vya nyuklia au mafuta vya Iran ili kuepusha vita vipana.

Kulingana na ripoti ya jana Jumatatu ya gazeti la Washington Post iliyowanukuu maafisa ambao hawakutajwa majina wa Marekani, Netanyahu aliihakikishia Ikulu ya Marekani kuwa Israel ilikuwa ikiwazia tu kulenga maeneo ya kijeshi.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa ofisi ya Netanyahu leo Jumanne ilielezea vinginevyo.

“Tunasikiliza maoni ya Marekani, lakini tutafanya uamuzi wetu wa mwisho kwa kuzingatia maslahi yetu ya taifa,” ilisema taarifa hiyo.

Share This Article