Israel na Hamas wakamilisha awamu ya 6 ya ubadilishanaji mateka

Mpango wa kusitisha vita na kubadilishana wafungwa ulianza kutekelezwa Januari 15, 2025.

Marion Bosire
2 Min Read

Israel na Hamas wamekamilisha awamu ya 6 ya ubadilishanaji wa mateka wa vita ambapo raia watatu wa Israel waliokuwa wamezuiliwa Gaza waliachiliwa na wapalestina 369 wakaachiliwa kutoka Israel.

Wapalestina wanne kati ya walioachiliwa huru wako katika hali mbaya na wamelazwa hospitalini na ripoti zinaashiria kwamba wanajeshi wa Israel waliwadhulumu hadi wakati wa kuachiliwa.

Waziri wa masuala ya kigeni nchini Marekani Marco Rubio aliwasili jijini Tel Aviv katika ziara yake ya siku 6 ya eneo la Mashariki ya Kati kujadili maendeleo ya mpango wa kusitisha vita.

Kulingana na takwimu za wizara ya afya ya Gaza, watu 48,239 waliuawa katika vita vya Israel huko Gaza, na wengine 111,676 wakajeruhiwa.

Chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali kiliripoti kwamba idadi hiyo ya vifo iliongezeka hadi elfu 61,709 kwani watu wengi ambao hawajulikani walipo wakichukuliwa kuwa wameaga dunia.

Shambulizi la Hamas nchini Israel Oktoba 7, 2023 ndilo lilianzisha vita hivyo na siku hiyo watu 1,139 waliuawa nchini Israel na zaidi ya 200 wakashikwa mateka.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anashikilia kwamba mpango unaoendelea kutekelezwa wa kusitisha vita ni lazima udumishwe na amekataa mipango ya kuhamisha wapalestina kutoka ardhi yao.

Matamshi yake yanafuatia pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kutwaa eneo la Gaza kwa ajili ya kulijenga upya na hivyo kulazimisha wapalestina kuhama.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *