Israel, Marekani na Hamas waripotiwa kuafikia makubaliano ya kusitisha vita kwa muda

Marion Bosire
1 Min Read

Israel, Marekani na Hamas wanaripotiwa kuafikia makubaliano ambayo yatatoa fursa ya kuachiliwa kwa wanawake na watoto walioshikwa mateka katika Ukanda wa Gaza na kusitishwa kwa vita katika eneo hilo kwa muda wa siku 5.

Haya ni kwa mujibu wa gazeti la the Washington Post Jumamosi, Novemba 18, 2023, ambalo lilinukuu watu wanaofahamu zaidi kuhusu mapatano hayo.

Kulingana na mapatano hayo ya kurasa 6, pande zote zinazohusika na mzozo huo zitasitisha mapigano kabisa kwa muda wa siku 5 huku mateka wakiachiliwa kwa idadi ndogo ndogo kila siku.

Kundi la Hamas liliteka nyara watu wapatao 240 kutoka Israel mnamo Oktoba 7, 2023 wakati lilivamia miji kadhaa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200.

Katika makubaliano hayo, ilikubaliwa kwamba ufuatiliaji wa angani utaendelea wakati wa kipindi hicho cha siku 5 ili kuhakikisha kwamba masharti ya mapatano yanatekelezwa.

Kipindi hicho cha siku 5 pia kitatumika kuwasilisha misaasa muhimu katika ukanda wa Gaza.

Ikulu ya Rais nchini Marekani na afisi ya waziri mkuu nchini Israel hazikutoa taarifa mara moja kuhusu mapatano hayo.

Inaaminika kwamba utekelezaji wa mapatano hayo huenda ukaanza hivi karibuni.

Share This Article