Iraq imelaani hatua ya Israel kutumia anga yake kuishambulia nchi jirani ya Iran katika barua ambayo imemwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN Antonio Guterres na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Nchi hiyo imeyasema hayo leo Jumatatu.
Taarifa kutoka kwa msemaji wa serikali Bassim Alawadi ilisema barua hiyo inalaani “ukiukaji mkubwa wa taifa hilo la Kiyahudi wa anga na uhuru wa kujitawala wa Iraq kwa kutumia anga ya Iraq kufanya shambulizi katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Oktoba 26”.
Alawadi amesema Wizara ya Mambo ya Nje itaibua suala la “ukiukaji huu” katika mazungumzo na Marekani, mshirika wa karibu na msambazaji nambari moja wa silaha wa Israel.
Juzi Jumamosi, Israel ilifanya mashambulizi ya anga katika vituo vya kijeshi vya Iran na kuongeza hatari ya mzozo wa kikanda kuzidi hata zaidi.
Hatua hiyo ikikuja zaidi ya mwaka mmoja wa vita katika eneo la Gaza na mwezi mmoja tangu kuzuka kwa vita kati ya Israel na kundi la Hezbollah nchini Lebanon.