Iran kufunga kabisa Mlango Bahari wa Hormuz iwapo Marekani itaishambulia

Marekani ilikuwa imeipa Iran makataa ya kufungua kabisa mlango huo au ishambulie vituo vyake vya kuzalisha umeme.

Marion Bosire
2 Min Read
Masoud Pezeshkian , Rais wa Iran

Iran imesema kwamba itafunga kabisa Mlango Bahari wa Hormuz iwapo Marekani itatekeleza tishio lake na kushambulia vituo vya nishati vya nchi hiyo iwapo haitafungua Mlango Bahari huo.

Rais Donald Trump wa Marekani alikuwa ameipa Iran makataa ya saa 48 kufungua Mlango Bahari huo muhimu kwa usafirishaji wa mafuta.

Kupitia mitandao ya kijamii, Trump amesema kwamba iwapo Iran itakosa kufungua eneo hilo katika muda huo, basi Marekani itashambulia na kuharibu kabisa vituo vyake muhimu vya kuzalisha umeme.

Iran nayo imepuuzilia mbali tishio hilo ikisema italenga miundombinu ya umeme na maji kote katika eneo la Mashariki ya Kati kama njia ya kulipiza kisasi iwapo tishio la Marekani litatimia.

Nchi zitakazolengwa na Iran katika shambulizi hilo ni zile ambazo ni wenyeji wa wanajeshi wa Marekani.

Vita katika eneo la Mashariki ya Kati vimeingia juma la nne sasa na hakuna dalili kwamba huenda vikakomeshwa hivi karibuni.

Vikosi vya Israel vimelipua daraja la Qasimiyah kusini mwa Lebanon, katika shambulio ambalo Rais Joseph Aoun anasema ni utangulizi wa uvamizi wa ardhini.

Vikosi vya Marekani na Israel vinaendelea kushambulia Iran huku jeshi la Israel likidaka makombora zaidi ya Iran.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameahidi kuiangamiza Iran baada ya shambulio lililowajeruhi watu zaidi ya 180 katika miji ya Arad na Dimona.

Share This Article