Halmashauri ya kutathmini utendakazi wa polisi, IPOA imekashifu vikali mashambulizi yaliyotekelezwa dhidi ya maafisa wa polisi, katika eneo la Banane, kaunti ya Garissa jana Alhamisi.
Kupitia kwa taarifa, mwenyekiti wa IPOA Anne Makori, alimtaka Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome kukabiliana vilivyo na wahalifu katika eneo hilo la Banane, huku akiwatakia afueni ya haraka maafisa wa polisi waliojeruhiwa.
“IPOA inasimama na Inspekta Mkuu wa Polisi pamoja na maafisa wote wa huduma ya taifa ya polisi wanapotekeleza majukumu yao ya kuwahakikishia Wakenya usalama,” alisema Makori kupitia kwa taarifa.
Aidha Makori alionya dhidi ya kushambuliwa kwa maafisa wa polisi walio kazini, akitaja hatua hiyo kuwa sawia na kuhujumu uhuru wa taifa hili.
Jana Alhamisi, afisa mmoja wa polisi wa kikosi cha GSU alijeruhiwa na wengine kadhaa kunusurika bila majeraha baada ya gari lao kushambuliwa na vilipuzi katika eneo la Banane, kaunti ya Garissa.
Maafisa hao walikuwa safarini kuelekea Hargadera kuwachukua maafisa wenzao ambao hawakuwa kazini wakati shambulizi hilo lilipotekelezwa.
Mwezi Novemba mwaka uliopita, maafisa wa polisi wanne waliuawa baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi kilichokuwa kimetegwa kwenye barabara ya Dadaab-Fafi walipokuwa kwenye doria ya kawaida.