IPOA yaeleza masharti ya matumizi ya nguvu ya polisi

Tom Mathinji
2 Min Read

Kufuatia kifo cha Rex Kanyeki Masai baada ya kupigwa risasi na afisa wa polisi Alhamisi jioni kwenye maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) imeeleza masharti kuhusu matumizi ya nguvu kulingana na Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na amri za kudumu za huduma.

Maafisa wa polisi hapa nchini, wamekuwa wakilaumiwa na wanaharakati wa haki za binamu kutokana na wao kutumia nguvu kupita kiasi kwa waandamanaji.

IPOA kupitia taarifa siku ya Ijumaa ilisema kuwa afisa wa polisi lazima wakati wowote ajaribu kutumia njia zisizo za vurugu.

Mamlaka hiyo ilisema kuwa kulingana na sheria ni kinyume kwa polisi kutumia nguvu kwa kisingizio kuwa anafuata amri za mkuu wake.

IPOA ilisema afisa wa polisi anayetumia aina yoyote ya nguvu ataripoti mara moja kwa mkuu wake.

Kulingana na IPOA, iwapo matumizi ya nguvu yatasababisha majeraha, maafisa wa polisi waliopo watatoa usaidizi wa kimatibabu mara moja ila ikiwa kuna sababu za msingi.

Kukosa kufanya hivyo, itachukuliwa kama kosa la jinai.

Katika hali ambapo matumizi ya nguvu itasababisha kifo, majeraha makubwa na matokeo mengine mabaya, IPOA ilisema itaripotiwa kwa mamlaka mara moja.

“Itakuwa ni kosa la kinidhamu kwa afisa wa polisi kukosa kuripoti kwa mujibu wa kanuni hizi,” ilisema IPOA.

IPOA ilibainisha kuwa afisa wa polisi aliyevalia sare wakati wote ataweka nembo ya jina au nambari ya Huduma inayoweza kutambulika katika sehemu inayoonekana wazi ya sare hiyo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *