Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini, IEBC imelaani mauaji ya kaimu meneja wa uchaguzi katika kaunti ya Kilifi Aisha Akinyi Abubakar.
Ripoti zinaashiria kwamba Aisha alishambuliwa katika makazi yake huko Utange, eneo bunge la Kisauni kaunti ya Mombasa usiku wa Januari 4, 2025.
Aliuawa kwenye shambulizi hilo huku mwanawe wa kiume akiachwa na majeraha mabaya na anapokea matibabu.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Afisa Mtendaji Marjan Hussein Marjan, IEBC imesikitishwa na tukio hilo huku ikitoa rambirambi zake kwa familia ya Aisha, marafiki na hata wafanyakazi wenza.
Tume hiyo imelaani mauaji hayo na kutaka uchunguzi wa kina utekelezwe na mashirika husika ya serikali ili wahusika wachukuliwe hatua na haki ipatikane.
Aisha Akinyi Abubakar amekuwa akifanya kazi na tume ya IEBC tangu mwaka 2012 ambapo alianza kama mshirikishi wa uchaguzi wa eneo bunge la Nyali na baadaye katika eneo bunge la Kilifi Kusini.
Alikuwa anafahamika sana kwa uadilifu, utaalamu na kujitolea kwa kazi yake. Tume ya IEBC imeapa kusaidia familia yake wakati huu wa majonzi.