Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka (IEBC), imesema usajili endelevu wa wapiga kura katika Eneo Bunge la Ol Kalaou umesimamishwa kufuatia kifo cha mbunge wa eneo hilo David Kiaraho.
Kifo cha mbunge Kiaraho kilitangazwa siku ya Jumapili na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, akisema mbunge huyo alifariki akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi.
Akizungumza alipozindua usajili endelevu wa wapiga katika eneo la Shimoni kaunti ya Kwale, mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon, alisema tume hiyo itatangaza tarehe mpya ambayo shughuli hiyo itatekelezwa baada ya kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo.
Ethakon alidokeza kuwa tume hiyo itaafikia lengo lake la kuwasajili wapiga kura wapya milioni 2.5, hususan kutokana na juhudi za vijana za kujisajili kwa wingi kuwa wapiga kura.
IEBC imewatuma maafisa wa usajili 12,000 katika zaidi ya vituo 30,000, ikilenga wapiga kura wapya milioni 2.5 million, taifa hili linapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Tume hiyo imesema itashirikiana na asasi zingine kuhakikisha hakuna mkenya aliyehitimu kusajiliwa anafungiwa nje.