Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka hapa nchini IEBC, imesema inahitaji shilingi bilioni 61.7 kuandaa Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2027.
Tume hiyo ikiongozwa na naibu katibu wake Obadiah Keitany, aliyemwakilisha Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Marjan Hussein Marjan mbele ya kamati ya bunge la taifa kuhusu hak na maswala ya sheria, ilisema inahitaji shilingi bilioni 55 kuandaa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, na pia inakabiliwa na nakisi ya shilingi bilioni 6.7 na madeni ambayo hayajalipwa ya shilingi bilioni 3.8.
Keitany alidokeza kuwa tume hiyo inapendekeza bajeti ya Uchaguzi Mkuu ifadhiliwe katika muda wa miaka mitatu ya kifedha kuanzia mwaka wa kifedha wa 2025/2026, ili kushughulikia shughuli za kabla ya Uchaguzi Mkuu kama vile usajili wa wapiga kura na ununuzi wa vifaa vya kidijitali vya uchaguzi.
Katibu huyo alifahamisha kamati hiyo ya bunge kuwa kuna chaguzi ndogo 14 ambazo zinatarajiwa kufanywa punde tu tume hiyo itakapowapata makamishna, huku maandalizi yake yakitarajiwa kugharimu shilingi bilioni 480.
“IEBC inatarajiwa kuandaa chaguzi ndogo punde tu tume hiyo itawapata makamishna na inahitaji rasilimali kutekeleza zoezi hilo. Kwa sasa kuna nafasi 14 ambazo ziko wazi, zikiwa ni pamoja na Seneta (1), Wabunge la taifa (4) na wawakilishi wadi (9),” alisema Keitany.
Tume ya IEBC imesema inalenga kuwasajili wapiga kura milioni 5.7 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, na kufikisha milioni 28 idadi jumla ya wapiga kura hapa nchini.