Idara ya Mahakama yamuomboleza hakimu Monica Kivuti

Tom Mathinji
2 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome (kulia) Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu (katikati) na Msajili wa idara ya Mahakama Winfridah Mokaya (Kushoto).

Idara ya mahakama siku ya Jumanne, ilimuomboleza hakimu mwandamizi wa Mahakama ya Makadara Monica Kivuti, aliyeuawa kwa kupigwa risasi wiki iliyopita akiwa kazini.

Katika kaunti ya Nairobi Jaji Mkuu Martha Koome, naibu wake Philomena Mwilu na msajili wa idara ya Mahakama  Winfridah Mokaya, waliwaongoza wafanyakazi wa idara hiyo katika mahakama za Makadara kumuomboleza hakimu huyo.

Jaji Mkuu Martha Koome aliwahakikishia maafisa wote wa mahakama, watumizi wa mahakama na wananchi kwa jumla kwamba usalama wao unasalia kupewa kipaumbele na utaimarishwa.

Koome alisema mauaji dhidi ya afisa wa idara ya Mahakama ni sawa na kushambulia uhuru wa idara ya mahakama.

“Leo tunahuzuni sana. Kama taasisi mioyo yetu imedhoofika, lakini nyoyo zetu ziko imara,” alisema Jaji Mkuu Martha Koome.

Kwa upande wake, naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu aliwataka wale ambao hawajaridhishwa na utendakazi wa maafisa wa idara ya mahakama, kuwa ripoti katika tume ya kuwaajiri wafanyakazi wa mahakama JSC, kuhakikisha wanaondolewa afisini.

“Iwapo tumekosea, usituue. Tushtaki katika tume ya kuwaajiri maafisa wa idara ya Mahakama JSC na utoe ushahidi wa kutosha, kuhakikisha tunaondolewa afisini,” alisema Mwilu aliyekuwa amejawa na majonzi.

Mwilu alitaka walio na jukumu la kuhakikisha usalama, kufanya hivyo kikamilifu.

“Tuache kuzungumza tu, ni wakati wa kuchukua hatua,” aliongeza Mwilu.

Kivuti aliaga dunia kutokana na majeraha ya risasi baada ya kushambuliwa na afisa mmoja wa polisi  wiki iliyopita katika mahakama ya Makadara.

Jaji mkuu ameliagiza mahakama zote kote nchini kurejelea vikao vyao leo sisipokuwa mahakama ya Makadara inayofanyiwa ukarabati kwasababu za kiusalama.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *