Idara ya mahakama yalaani kunyanyaswa kwa wanahabari

Martin Mwanje
1 Min Read

Idara ya mahakama imeshutumu vikali kudhulumiwa kwa wanahabari katika majengo ya mahakama ya Milimani. 

Hii ni baada ya maafisa wa polisi kunaswa kwenye picha ya video wakiwanyanyasa wanahabari waliokuwa wakifuatilia kesi iliyomkabili mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.

“Nadhari ya idara ya mahakama imevutiwa na picha ya video inayosambaa katika baadhi ya vyombo vya habari ikiwaonyesha polisi wakiwanyanyasa wanahabari waliokuwa wakifuatilia taarifa katika mahakama ya Milimani,” inaelezea taarifa iliyotumwa na Ukurugenzi wa Masuala ya Umma na Mawasiliano wa Idara ya Mahakama leo Ijumaa alasiri.

“Uhuru wa vyombo vya habari umelindwa chini ya Kifungu Namba 34 cha Katiba ya Kenya ya mwaka 2010. Tunalaani vikali kunyanyaswa kwa vyombo vya habari wakati vikitekeleza majukumu yao, kokote na hasa ndani ya majengo ya mahakama.”

Idara ya Mahakama inasema inawatarajia watu wote, hasa washirika wa sekta ya haki, kuonyesha viwango vya juu vya mienendo katika vyumba vya mahakama na ndani ya majengo ya mahakama.

“Mienendo ya wadau wote wa haki inapaswa wakati wote kuhamasisha na kudumisha utawala wa sheria na kujenga imani ya umma katika mfumo wa mahakama,” iliongeza taarifa hiyo.

Idara ya Mahakama imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari, haki za wanahabari na utawala wa sheria.

Website |  + posts
Share This Article