Idadi ya raia wa kigeni ambao wametuma maombi ya kuzuru taifa hili kupitia mfumo mpya wa kielektoniki, imefika 132,000 katika muda wa wiki moja iliyopita.
Kulingana na takwimu kutoka idara ya uhamiaji hapa nchini, maombi ya raia 25,000 wanaotaka kuzuru Kenya yameidhinishwa, huku maombi 110 yakikatiliwa kutokana na maswala ya kiusalama.
Katibu katika idara ya uhamiaji na huduma kwa wananchi Julius Bitok, amesema Kenya imeweza kukusanya zaidi ya shilingi milioni 156 katika kipindi cha wiki moja iliyopita kufuatia kuanzishwa kwa mfumo huo wa kielektroniki wa kuidhinisha usafiri humu nchini.
Kulingana na Bitok, mfumo huo mpya uliozinduliwa umeongeza idadi ya wasafiri wanaozuru humu nchini.
“Tumeweza kukusanya dola milioni moja katika muda wa wiki moja iliyopita. Idadi ya watalii wanaozuru nchi hii imeongezeka, kwa sababu tumerahisisha usafiri wa kuingia hapa nchini,” alisema Bitok.
Katibu huyo ambaye alizungumza wakati wa ziara yake katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA alisema mfumo huo umeiwezesha serikali kukusanya deta kuhusu wale wanaozuru humu nchini ambapo haingefanikishwa na mfumo uliokuwa umelemazwa.
Aidha, Bitok alisema hakuna mrundiko kwa vile mfumo huo ni madhubuti kwa sababu una uwezo wa kuwachagua wale wanaohitaji kukaguliwa zaidi katika juhudi za kushughulikia masuala ya ki-usalama.
Bitok ambaye alikuwa ameandamana na mkurugenzi mkuu wa uhamiaji Evelny Cheluget alikariri kwamba kutokana na mfumo huo mpya,idadi ya raia watakaozuru hapa nchini itazidi kuongezeka,hivyo basi kupiga jeki sekta ya utalii humu nchini.