Idadi ya raia wa kigeni wanaowasili nchini yaongezeka kwa asilimia 18.42

Tom Mathinji
1 Min Read
Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura.

Serikali imetangaza kuimarika kwa sekta ya utalii, huku idadi ya raia ya kigeni wanaoingia humu nchini ikiongezeka kwa asilimia 18.42.

Akizungumza siku ya Alhamisi, msemaji wa serikali Isaac Mwaura, alisema sekta ya utalii imeandikisha ukuaji wa shilingi milioni 650 kutokana na ongezeko za safari na matumizi ya utalii hapa nchini.

Mwaura alidokeza ukuaji huo pia ulichangiwa pakubwa na hatua ya serikali ya kuondoa hitaji la visa kuingia hapa nchini kwa raia wa kigeni, akisema taifa hili linazidi kuwavutia watalii wengi.

“Idadi ya siku ambazo watalii huwa humu nchini imeongezeka kutoka siku 10 hadi siku 11, na jinsi wanavyokaa humu nchini, ndivyo wanatumia fedha zaidi katika mikahawa,” alisema Mwaura.

Aidha alisema ukuaji huo pia ulitokana na ongezeko la mikutano, makongano na maonyesho ya bidhaa, ambapo idadi ya wasafiri wa kimataifa ilifika 10,000, huku mikutano ya kimataifa hapa nchini ikongezeka hadi 2,151 na zaidi ya wageni 14,000 wakihudhuria mikutano hiyo kutoka kote ulimwenguni.

Aliongeza kuwa serikali imeongeza idadi ya fursa za mafunzo kwa zaidi vijana 1,044 chini ya serikali ya Kenya Kwanza, ambao watasaidia kukuza uchumi wa taifa.

TAGGED:
Share This Article